4 Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”
5 Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi
6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.”
7 Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.”
8 Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.
9 Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.”
10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii.