1 Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake.
2 Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.”
3 Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!”
4 Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu?
5 Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’
6 Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.”