1 Kisha, nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.
2 Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi kavu,
3 na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.
4 Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!”
5 Kisha, yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
6 akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!