26 Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Kristo kuna faida kubwa kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.
27 Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.
28 Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.
29 Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.
30 Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba.
31 Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.
32 Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii.