1 Ndugu zangu, watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu Mtume na Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama.
2 Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
3 Lakini Yesu anastahili heshima kubwa kuliko Mose maana mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe.
4 Kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.
5 Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye.
6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi wenyewe ni nyumba yake kama tukiendelea kuwa hodari na thabiti katika kile tunachotumainia.
7 Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu:“Kama mkisikia sauti yake leo,
8 msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasikama wakati ule wa majaribio kule jangwani.
9 Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza,ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini!
10 Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema,‘Fikira za watu hawa zimepotoka,hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’.
11 Basi, nilikasirika, nikaapa:‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’
12 Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai.
13 Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.
14 Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
15 Maandiko yasema hivi:“Kama mkisikia sauti yake leo,msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi.”
16 Ni akina nani waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri.
17 Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arubaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani.
18 Mungu alipoapa: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko,” alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi.
19 Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.