1 Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu.
2 Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani.
3 Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.”
4 Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
5 Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,