1 Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea, hata kama wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2 Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki.
3 Lakini wewe rafiki unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo hali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
4 Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?
5 Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa.
6 Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
7 Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele.