11 Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu.
12 Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi.
13 Kabla ya sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria.
14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu.Adamu alikuwa kielelezo cha Kristo ambaye alikuja baadaye.
15 Lakini kosa la Adamu haliwezi kulinganishwa na neema ya Mungu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake.
16 Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe.
17 Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.