17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
18 “Haya nisemayo hayawahusu nyinyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: ‘Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.’
19 Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa ‘Mimi Ndimi.’
20 Kweli nawaambieni: Anayempokea yule ninayemtuma ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.”
21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!”
22 Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani.
23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.