1 Solomoni alifanya ushirikiano na Farao mfalme wa Misri, kwa kumwoa binti yake. Akamleta binti Farao na kumweka katika mji wa Daudi, mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake mwenyewe, nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ukuta wa kuuzunguka mji wa Yerusalemu.
2 Kabla yake, watu walikuwa wakitoa tambiko vilimani, kwa kuwa nyumba ya Mungu ilikuwa bado haijajengwa.
3 Solomoni alimpenda Mwenyezi-Mungu, akazingatia maongozi ya Daudi, baba yake; ila tu, naye ilimbidi kutoa tambiko na kufukiza ubani vilimani.
4 Wakati mmoja, Solomoni alikwenda kutoa tambiko huko Gibeoni, maana palikuwa ndipo mahali maarufu pa ibada. Ilikuwa ni kawaida ya Solomoni kutoa maelfu ya sadaka za kuteketezwa katika madhabahu hiyo.
5 Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.”
6 Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi.
7 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu.