12 basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako.
13 Pia, nitakupa yale ambayo hukuomba: Nitakupa utajiri na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote wa nyakati zako.
14 Tena kama ukifuata njia na maagizo yangu na kushika amri zangu kama alivyofanya baba yako Daudi, basi, nitakupa maisha marefu.”
15 Solomoni alipoamka, alitambua kwamba ilikuwa ndoto. Ndipo akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, akamtolea tambiko za kuteketezwa na za amani. Halafu akawafanyia karamu watumishi wake wote.
16 Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni.
17 Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani.
18 Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu.