14 Walawi waliyaacha malisho yao, na maeneo yao mengine kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwakataza kumtumikia Mwenyezi-Mungu kama makuhani wa Mwenyezi-Mungu.
15 Yeroboamu alijichagulia makuhani wake mwenyewe wa kuhudumu mahali pa juu pa kuabudia miungu na yale majini na sanamu za ndama alizojitengenezea.
16 Watu wote ambao walikuwa wamenuia kwa moyo wa dhati kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kutoka katika makabila yote ya Israeli, waliandamana na Walawi hadi Yerusalemu ili wapate kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.
17 Hivyo, waliuimarisha ufalme wa Yuda, na kwa muda wa miaka mitatu, wakauunga mkono utawala wa Rehoboamu mwanawe Solomoni, nao ukawa imara na wakaishi katika hali ileile waliyoishi wakati walipokuwa chini ya utawala wa mfalme Daudi na mfalme Solomoni.
18 Rehoboamu alioa mke, jina lake Mahalathi binti Yeremothi mwana wa Daudi. Mama yake alikuwa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese.
19 Naye alimzalia wana watatu: Yeushi, Shemaria na Zahamu.
20 Baadaye, alimwoa Maaka binti Absalomu, naye akamzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi.