1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2 Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Uzia baba yake; isipokuwa yeye hakuingia katika hekalu la Mwenyezi-Mungu nao watu waliendelea kufanya maovu.
3 Yothamu alijenga Lango la Kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kushughulika sana na ujenzi wa ukuta sehemu ya Ofeli.
4 Alijenga miji kwenye nchi ya milima ya Yuda, na kwenye misitu, akajenga ngome na minara katika milima yenye misitu.
5 Alipigana vita dhidi ya mfalme wa Amoni na kuwashinda. Katika mwaka huo Waamoni walimtolea ushuru wa kilo 3,400, tani 1,000 za ngano na kilo 1,000 za shayiri; waliendelea kufanya hivyo katika mwaka wa pili na wa tatu.
6 Mfalme Yothamu aliendelea kuwa mwenye nguvu, kwa sababu aliishi kwa kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
7 Matendo mengine ya Yothamu, vita vyake na maongozi yake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Habari za Wafalme wa Israeli na Yuda.
8 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu.
9 Alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.