1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa utawala wa mfalme Asa, Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga mji wa Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.
2 Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, akazituma Damasko kwa Ben-hadadi, mfalme wa Aramu na ujumbe akasema,
3 “Na tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama nakupa zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli ili aache mashambulizi dhidi yangu.”
4 Hapo mfalme Ben-hadadi alikubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao waliiteka miji ya Iyoni, Dani, Abel-maimu, na miji yote ya Naftali iliyokuwa na ghala za vyakula.
5 Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo, aliacha kuujenga mji wa Rama, akasimamisha kazi yake.
6 Ndipo mfalme Asa alipowapeleka watu wote wa Yuda, wakahamisha mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha Asa alitumia vifaa hivyo kujengea miji ya Geba na Mizpa.
7 Wakati huo, Hanani mwonaji alimwendea mfalme Asa wa Yuda, akamwambia, “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Shamu badala ya kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, jeshi la mfalme wa Shamu limekuponyoka.
8 Je, wale Waethiopia na Walibia hawakuwa jeshi kubwa na magari na wapandafarasi wengi? Lakini kwa vile ulimtegemea Mwenyezi-Mungu, yeye aliwatia mikononi mwako.
9 Mwenyezi-Mungu huuchunga kwa makini ulimwengu wote, ili kuwapa nguvu wale walio waaminifu kwake. Umetenda jambo la kipumbavu, kwa hiyo tangu sasa, utakuwa na vita kila mara.”
10 Maneno haya yalimfanya Asa amkasirikie sana Hanani mwonaji, hata akamfunga gerezani. Wakati huohuo, Asa alianza kuwatesa vikali baadhi ya watu.
11 Matendo ya Asa, toka mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha “Wafalme wa Yuda na Israeli.”
12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa ufalme wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu, akaugua sana. Lakini hata wakati huo, Asa hakumgeukia Mwenyezi-Mungu amsaidie, bali alijitafutia msaada kutoka kwa waganga.
13 Hatimaye Asa alifariki mnamo mwaka wa arubaini na moja wa utawala wake.
14 Alizikwa katika kaburi alilokuwa amejichimbia mwenyewe mwambani, katika mji wa Daudi. Walimlaza ndani ya jeneza lililokuwa limejazwa manukato ya kila aina yaliyotayarishwa na mafundi wa kutengeneza marashi, wakawasha moto mkubwa sana kwa heshima yake.