1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia kutoka Beer-sheba.
2 Wakati wote kuhani Yehoyada alipokuwa hai Yoashi alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu.
3 Yehoyada akamwoza wake wawili, nao wakamzalia watoto wa kiume na wa kike.
4 Baadaye Yoashi aliamua kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
5 Basi, akawaita makuhani na Walawi na kuwaamuru, “Nendeni katika miji ya Yuda, mkusanye fedha kutoka kwa Waisraeli wote ili kurekebisha nyumba ya Mungu wenu kila mwaka; harakisheni.” Lakini Walawi hawakuharakisha.
6 Basi, mfalme akamwita kiongozi Yehoyada, akamwuliza, “Mbona hujaamrisha Walawi kukusanya kutoka kwa watu wa Yuda na Yerusalemu, kodi ambayo Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliagiza watu walipe kwa ajili ya Hema Takatifu la Mwenyezi-Mungu?”