2 Mambo Ya Nyakati 24:9-15 BHN

9 Kisha tangazo likatolewa kote katika Yuda na Yerusalemu, kwamba watu wote wamletee Mwenyezi-Mungu kodi ambayo Mose mtumishi wa Mungu, aliwaamuru Waisraeli walipokuwa jangwani.

10 Wakuu wote na watu wote walifurahi wakaleta kodi yao wakaitumbukiza kwenye sanduku mpaka walipomaliza kufanya hivyo.

11 Walawi walipopeleka sanduku hilo kwa maofisa wa mfalme, nao walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani, katibu wa mfalme pamoja na mwakilishi wa kuhani mkuu, walizitoa sandukuni, kisha wakalirudisha mahali pake. Waliendelea kufanya hivyo kila siku, wakakusanya fedha nyingi.

12 Mfalme na Yehoyada walizitoa fedha hizo na kuwapa wale waliosimamia kazi ya urekebishaji wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao wakawaajiri waashi, maseremala warekebishe nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Waliajiri pia mafundi wa chuma na shaba ili kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

13 Hivyo mafundi hao walishughulika na kazi hiyo kwa bidii, wakairudisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika hali yake ya awali, wakaiimarisha.

14 Walipomaliza kuitengeneza nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walimletea mfalme na Yehoyada dhahabu na fedha iliyobaki; halafu vyombo kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vilitengenezwa kwa fedha hizo, vyombo hivyo vilikuwa vya kutumika katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, matoleo ya sadaka za kuteketeza na mabakuli ya kufukizia ubani, pia vyombo vya dhahabu na vya fedha. Watu waliendelea kutoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakati wote wa utawala wa Yehoyada.

15 Lakini Yehoyada alizeeka na alipofikisha umri wa miaka 130, alifariki.