14 Uzia aliwapa askari hao ngao, mikuki, kofia za chuma, deraya, pinde na mawe kwa ajili ya kupiga kwa kombeo.
15 Huko Yerusalemu mafundi wake walimtengenezea mitambo ya kurushia mishale na mawe makubwamakubwa. Sifa zake zilienea kila mahali, nguvu zake zikaongezeka zaidi kwa sababu ya msaada mwingi alioupata kutoka kwa Mungu.
16 Wakati mfalme Uzia alipokuwa na nguvu, alijaa kiburi ambacho kilisababisha maangamizi yake. Alimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wake kwa kuingia hekaluni akikusudia kufukiza ubani madhabahuni.
17 Lakini kuhani Azaria, pamoja na makuhani wengine mashujaa themanini, wakamfuata mfalme
18 na kumzuia. Wakamwambia, “Si wajibu wako hata kidogo Uzia, kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. Ni makuhani tu wa uzao wa Aroni ambao wamewekwa wakfu kufukiza ubani. Ondoka mahali hapa patakatifu. Umemkosea Mwenyezi-Mungu na hutapata heshima yoyote kutoka kwake.”
19 Wakati huo, Uzia alikuwa amesimama hekaluni karibu na madhabahu, ameshikilia chetezo cha kufukizia ubani mkononi. Aliwakasirikia makuhani; na mara alipofanya hivyo, akashikwa na ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani hao.
20 Azaria, kuhani mkuu, na wale makuhani wengine, walimtazama, kisha wakaharakisha kumtoa nje; hata yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwadhibu.