9 Baba zetu waliuawa vitani, na wana wetu na binti zetu na wake zetu ni mateka kwa sababu hiihii.
10 Sasa, nimeamua kwa dhati kufanya agano na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ili asitukasirikie zaidi.
11 Basi wanangu, muwe na nidhamu. Mwenyezi-Mungu amewachagua nyinyi ili mumtumikie, muwaongoze watu wake katika ibada, na kumfukizia ubani.”
12 Walawi wafuatao wakaanza kazi: Kutoka ukoo wa Kohathi walikuwa Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria; ukoo wa Merari: Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yehaleli; ukoo wa Gershoni: Yoa mwana wa Zima, na Edeni mwana wa Yoa;
13 ukoo wa Elisafani: Shimori na Yeneli,
14 ukoo wa Hemani: Zekaria na Matania; ukoo wa Yeduthuni: Shemaya na Uzieli.
15 Hawa waliwakusanya Walawi wenzao, wakajitakasa. Kisha wakaingia kama walivyotakiwa kufanya na mfalme, wakaanza kusafisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza.