2 Mfalme Solomoni alianza ujenzi wa hekalu mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa utawala wake.
3 Vipimo alivyotumia Solomoni katika ujenzi wa nyumba ya Mungu, vilikuwa kadiri ya vipimo vya awali, urefu mita 27 na upana mita 9.
4 Chumba cha sehemu ya kuingilia kilikuwa na urefu wa mita 9, sawa na upana wa nyumba hiyo, na kimo chake mita 54. Kuta zake zilifunikwa kwa dhahabu safi upande wa ndani.
5 Ukumbi ulizungushiwa mbao za miberoshi na kufunikwa kwa dhahabu safi na kuchorwa mifano ya miti ya mitende na minyororo.
6 Mfalme Solomoni aliipamba nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa mawe mazuri ya thamani. Dhahabu aliyotumia ilitoka nchi ya Parvaimu.
7 Aliifunika nyumba yote kwa dhahabu: Boriti zake, vizingiti vyake, kuta zake na milango yake. Kutani palichongwa viumbe wenye mabawa.
8 Tena, alipatengeneza mahali patakatifu sana. Urefu wake ulikuwa mita 9, sawasawa na upana wake ambao pia ulikuwa mita 9. Alitumia zaidi ya tani 20 za dhahabu kukifunika chumba hicho.