1 Mfalme Hezekia aliwatumia ujumbe watu wote wa Israeli na Yuda, na pia akawaandikia barua wenyeji wa Efraimu na Manase, akiwaalika wote waje katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu Yerusalemu, ili kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa heshima yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
2 Mfalme, viongozi na watu wote wa mji wa Yerusalemu waliafikiana kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka mnamo mwezi wa pili
3 badala ya mwezi wa kwanza kama ilivyokuwa kawaida, kwa sababu idadi ya makuhani waliokuwa wamekwisha kujiweka wakfu ilikuwa ndogo, nao watu walikuwa bado hawajakusanyika Yerusalemu.
4 Aidha, mpango huu ulimridhisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa wamekusanyika.
5 Kwa hiyo waliamua kutoa tangazo kote nchini Israeli, kutoka Beer-sheba hadi Dani, kwamba watu waje Yerusalemu kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Ulikuwa umepita muda mrefu kabla watu hawajaiadhimisha Pasaka kulingana na sheria zake.