10 “Hivi ndivyo anavyosema Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mnategemea nini hata mnakaa Yerusalemu, mji ambao umezingirwa?
11 Je, si kana kwamba Hezekia anawadanganya ili awafanye mfe kwa njaa au kiu anapowaambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawaokoa mikononi mwa mfalme wa Ashuru?’
12 Je, siye huyu Hezekia aliyepaharibu mahali pake pa kuabudia na madhabahu zake na kuwaamuru watu wote wa Yuda na Yerusalemu akisema: ‘Mtaabudu mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtateketeza sadaka zenu?’
13 Je, kwani hamjui yale yote ambayo mimi na babu zangu tumewatenda watu wote wa mataifa mengine? Je, miungu ya mataifa ya nchi hizo iliweza kuzikomboa nchi zao mkononi mwangu?
14 Ni mungu gani kati ya miungu ya mataifa hayo iliyoharibiwa kabisa na babu zangu aliyeweza kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwangu ndio nanyi muwe na tumaini ya kwamba Mungu wenu atawaokoeni mikononi mwangu?
15 Msidanganywe na Hezekia wala msishawishike kwa hayo. Msimwamini mtu huyu, kwa maana hapajatokea mungu wa taifa au mfalme yeyote aliyefaulu kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru, sembuse huyu Mungu wenu!”
16 Watumishi wa mfalme wa Ashuru walisema maneno mengine mengi mabaya dhidi ya Mwenyezi-Mungu, na dhidi ya Hezekia mtumishi wake.