16 Watumishi wa mfalme wa Ashuru walisema maneno mengine mengi mabaya dhidi ya Mwenyezi-Mungu, na dhidi ya Hezekia mtumishi wake.
17 Mfalme mwenyewe aliandika barua akamtukana na kumdharau Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kama vile ambavyo miungu ya mataifa mengine haikuweza kuwaokoa watu wao kutoka mikononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake.”
18 Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi.
19 Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu!
20 Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya.
21 Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga.
22 Kwa njia hii basi, Mwenyezi-Mungu akamwokoa mfalme Hezekia na wakazi wa Yerusalemu kutoka mkono wa Senakeribu mfalme wa Ashuru, na kutoka mkono wa maadui wake wote. Akawapa maisha ya amani na jirani zake wote.