5 Ili kuuhami mji, mfalme Hezekia alipiga moyo konde, akajenga upya ukuta wote uliokuwa umebomoka, na juu yake akajenga minara. Upande wa nje, akajenga ukuta mwingine wa pili, na akaiimarisha sehemu iliyoitwa Milo katika mji wa Daudi. Zaidi ya hayo alitengeneza silaha na ngao kwa wingi.
6 Aliwaweka watu wote mjini chini ya makamanda, kisha akawaamuru wakusanyike uwanjani penye Lango la Mji. Hapo akawatia moyo akisema,
7 “Muwe imara na hodari. Msiogope wala msifadhaike mbele ya mfalme wa Ashuru au majeshi yake maana tuliye naye ni mkuu kuliko aliye naye Senakeribu.
8 Yeye anazo nguvu za kibinadamu tu, hali sisi tunaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Maneno haya ya mfalme Hezekia yaliwatia moyo sana watu hao.
9 Baada ya hayo, Senakeribu mfalme wa Ashuru, ambaye bado alikuwa ameuzingira mji wa Lakishi akiwa na majeshi yake yote, aliwatuma watumishi wake Yerusalemu kwa Hezekia mfalme wa Yuda na kwa watu wote wa Yuda waliokuwa Yerusalemu, akisema
10 “Hivi ndivyo anavyosema Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mnategemea nini hata mnakaa Yerusalemu, mji ambao umezingirwa?
11 Je, si kana kwamba Hezekia anawadanganya ili awafanye mfe kwa njaa au kiu anapowaambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawaokoa mikononi mwa mfalme wa Ashuru?’