10 Lakini mfalme akamwambia, “Je, kuna nini kati yangu na nyinyi wana wa Seruya? Ikiwa Mwenyezi-Mungu amemwambia ‘Mlaani Daudi’, nani sasa anaweza kuuliza ‘Kwa nini umefanya hivyo?’”
11 Tena mfalme Daudi akamwambia Abishai na hata watumishi wake wote, “Ikiwa mtoto wangu mwenyewe anayawinda maisha yangu, je si zaidi mtu wa kabila la Benyamini? Nyinyi mwacheni anilaani kwani Mwenyezi-Mungu amemwagiza anilaani.
12 Huenda Mwenyezi-Mungu akaangalia uovu wangu, naye akanilipa wema kwa laana hii ninayopata leo.”
13 Hivyo mfalme Daudi na watu wake wakaendelea na safari huku Shimei akiwa anamfuata akimtupia mawe na kurusha juu vumbi dhidi ya mfalme Daudi. Shimei alikuwa akitembea kileleni mwa mlima, mkabala na mfalme Daudi.
14 Kisha mfalme pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakafika mtoni wakiwa wamechoka. Basi wakapumzika.
15 Wakati huo, Absalomu na watu wote wa Israeli wakaenda mjini Yerusalemu na Ahithofeli pamoja nao.
16 Hushai kutoka Arki, rafiki ya Daudi, akamwendea Absalomu, akamwambia, “Uishi mfalme! Uishi mfalme!”