4 Mfalme akamwambia Siba, “Basi, yale yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akamwambia, “Nashukuru, bwana wangu mfalme, nami naomba nipate fadhili mbele yako daima.”
5 Wakati Daudi alipowasili kule Bahurimu, alitokea mtu mmoja wa ukoo wa Shauli, jina lake Shimei mwana wa Gera, akaanza kumlaani Daudi kwa mfululizo.
6 Akawa anamtupia mfalme Daudi mawe pamoja na watumishi wake. Watu wengine wote na mashujaa wakawa wanamzunguka Daudi upande wa kulia na kushoto.
7 Shimei alimlaani Daudi akisema, “Nenda zako; nenda zako, wewe mtu mwuaji, mtu asiye na faida!
8 Mwenyezi-Mungu amekulipiza kisasi kutokana na kumwaga damu yote ya jamaa ya Shauli, ambaye sasa wewe umechukua ufalme mahali pake. Sasa, Mwenyezi-Mungu amempa ufalme Absalomu mwanao. Tazama, sasa maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mwuaji.”
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu akulaani wewe bwana wangu mfalme? Niruhusu nimwendee, nami nitakikata kichwa chake.”
10 Lakini mfalme akamwambia, “Je, kuna nini kati yangu na nyinyi wana wa Seruya? Ikiwa Mwenyezi-Mungu amemwambia ‘Mlaani Daudi’, nani sasa anaweza kuuliza ‘Kwa nini umefanya hivyo?’”