9 Watu wote walikuwa wanashindana wao kwa wao katika makabila yote ya Israeli, wakisema, “Mfalme Daudi alitukomboa mikononi mwa adui zetu, alituokoa mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa ameikimbia nchi, akimkimbia Absalomu.
10 Tena Absalomu ambaye tulimpaka mafuta awe mfalme wetu, sasa ameuawa vitani. Sasa, kwa nini hatuzungumzii juu ya kumrudisha mfalme Daudi?”
11 Mfalme Daudi akatuma ujumbe kwa makuhani Sadoki na Abiathari, “Waambieni wazee wa Yuda: ‘Kwa nini wao wawe ndio wa mwisho kumrudisha mfalme nyumbani kwake? Ujumbe wa Israeli yote umenifikia mimi mfalme.
12 Nyinyi ni ndugu zangu, nyinyi ni damu yangu; kwa nini muwe wa mwisho kunirudisha mimi mfalme nyumbani?
13 Mwulizeni pia Amasa kama yeye si damu yangu. Tena Mungu aniue ikiwa simfanyi yeye kuwa kamanda wa jeshi langu tangu leo badala ya Yoabu.’”
14 Hivyo, Daudi aliivuta mioyo ya watu wote wa Yuda kama mtu mmoja. Hivyo, wakampelekea ujumbe kusema “Rudi nyumbani, wewe na watumishi wako wote.”
15 Basi, mfalme akaja mto Yordani na watu wote wa Yuda wakaja mpaka Gilgali kumlaki mfalme na kumvusha mtoni Yordani.