14 Daudi pia alituma wajumbe kwa Ishboshethi mwana wa Shauli akisema, “Nirudishie mke wangu Mikali ambaye nilimwoa kwa magovi 100 ya Wafilisti.”
15 Basi, Ishboshethi alituma watu wakamchukue Mikali kutoka kwa mumewe, Paltieli mwana wa Laishi.
16 Lakini Paltieli akaenda pamoja na mkewe huku analia njia nzima mpaka huko Bahurimu. Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani.” Naye akarudi.
17 Abneri alifanya mashauri na wazee wa Israeli, akawaambia, “Kwa muda fulani uliopita mmekuwa mkitaka Daudi awe mfalme wenu.
18 Sasa, lileteni jambo hilo hadharani kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwahidi hivi Daudi, ‘Kwa mkono wako wewe Daudi mtumishi wangu, nitawaokoa watu wangu wa Israeli kutoka kwa Wafilisti na kutoka kwa adui zao wengine.’”
19 Abneri pia akazungumza na Wabenyamini, kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kuhusu yale ambayo watu wote wa Israeli na kabila lote la Benyamini walipatana kutenda.
20 Abneri alipomwendea Daudi, alikuwa na watu ishirini, Daudi aliwafanyia karamu.