4 Adoniya, mzaliwa wake wa nne, mama yake alikuwa Hagithi; Shefatia, mzaliwa wake wa tano, mama yake alikuwa Abitali,
5 na Ithreamu, mzaliwa wake wa sita, mama yake alikuwa Egla, mke wake Daudi. Daudi alizaliwa wana hawa wote alipokuwa huko Hebroni.
6 Kadiri vita vilivyoendelea kati ya jamaa ya Daudi na ile ya Shauli, Abneri alizidi kujiimarisha katika jamaa ya Shauli.
7 Shauli alikuwa na suria mmoja aitwaye Rispa, binti Aya. Basi, wakati mmoja, Ishboshethi akamwuliza Abneri, “Kwa nini umelala na suria wa baba yangu?”
8 Abneri alikasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi, akasema: “Je, unafikiri mimi naweza kumsaliti Shauli? Je, unafikiri kuwa mimi naitumikia jamaa ya Yuda? Tazama, mimi nimekuwa mtiifu kwa jamaa ya baba yako Shauli, ndugu zake, rafiki zake na sijakutia mikononi mwa Daudi hadi leo. Hata hivyo, leo hii unaniona kuwa mwenye hatia kwa ajili ya mwanamke.
9 Mungu aniue ikiwa sitatekeleza yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi.
10 Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kuwa atauhamisha ufalme kutoka jamaa ya Shauli na kumpa yeye. Naye atatawala Israeli na Yuda kutoka Dani hadi Beer-sheba.”