3 Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.”
4 Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani,
5 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa?
6 Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani.
7 Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi?
8 Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli.
9 Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani.