7 Daudi alizichukua ngao za dhahabu walizobeba wanajeshi wa Hadadezeri na kuzipeleka Yerusalemu.
8 Pia alichukua shaba nyingi sana kutoka miji ya Beta na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri.
9 Wakati Toi, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,
10 alimtuma mwanawe Yoramu kwa mfalme Daudi kumpelekea salamu na pongezi kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri na kumshinda. Maana Hadadezeri alipigana na Toi mara nyingi. Yoramu alimpelekea Daudi zawadi za vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.
11 Zawadi hizo, pamoja na fedha na dhahabu alizokuwa ameziteka kwa mataifa yote aliyoyashinda, aliziweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu,
12 yaani kutoka Edomu, Moabu, Amoni, Filistia, Amaleki, pamoja na nyara alizoteka kwa mfalme Hadadezeri, mwana wa Rehobu mfalme wa Soba.
13 Daudi alijiongezea umaarufu wake. Alipokuwa anarudi baada ya kumshinda Hadadezeri, aliwaua Waedomu 18,000, katika Bonde la Chumvi.