30 Meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye atashikwa na hofu. Kisha atarudi nyuma huku amejaa hasira na atalitangua agano takatifu. Hapo atafuata shauri la wale walioasi agano takatifu.
31 Wanajeshi wake watalitia najisi hekalu na ngome zake, watakomesha tambiko za kuteketezwa kila siku na kusimamisha huko hekaluni chukizo haribifu.
32 Atawashawishi kwa hila wale walioasi agano, lakini watu walio waaminifu kwa Mungu wao watasimama imara na kuchukua hatua.
33 Wenye hekima miongoni mwa watu watawafundisha wengi. Hata hivyo, kwa siku kadhaa watauawa kwa upanga au moto, watachukuliwa mateka au kunyanganywa mali zao.
34 Wakati wanapouawa, watapata msaada kidogo, na wengi wanaojiunga nao, watafanya hivyo kwa unafiki.
35 Baadhi ya wenye hekima watauawa, ili wapate kuondolewa uchafu, kutakaswa na kusafishwa, mpaka wakati wa mwisho, ambao sasa bado haujatimia.
36 “ ‘Mfalme atafanya kama apendavyo. Atajitukuza na kujikweza kwamba yeye ni mkuu kuliko miungu yote, na kumkufuru Mungu wa miungu. Ataendelea kufanikiwa mpaka ghadhabu ifikie kikomo chake, kwani yaliyopangwa lazima yatimie.