34 Wakati wanapouawa, watapata msaada kidogo, na wengi wanaojiunga nao, watafanya hivyo kwa unafiki.
35 Baadhi ya wenye hekima watauawa, ili wapate kuondolewa uchafu, kutakaswa na kusafishwa, mpaka wakati wa mwisho, ambao sasa bado haujatimia.
36 “ ‘Mfalme atafanya kama apendavyo. Atajitukuza na kujikweza kwamba yeye ni mkuu kuliko miungu yote, na kumkufuru Mungu wa miungu. Ataendelea kufanikiwa mpaka ghadhabu ifikie kikomo chake, kwani yaliyopangwa lazima yatimie.
37 Mfalme huyo hataijali miungu ya wazee wake wala yule anayependwa na wanawake. Ataidharau miungu mingine yote, kwani atajiweka kuwa mkuu kuliko kila mmoja wao.
38 Badala ya miungu hiyo atamheshimu mungu mlinzi wa ngome, ambaye wazee wake kamwe hawakumwabudu, atamtolea dhahabu, fedha na vito vya thamani, na zawadi za thamana kubwa.
39 Atazishughulikia ngome zake kwa msaada wa mungu wa kigeni. Wale wanaomtambua kuwa mfalme, atawatunukia heshima kubwa, atawapa vyeo vikubwa na kuwagawia ardhi kama zawadi.
40 “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji.