7 Baadaye, mmojawapo wa ukoo wa huyo binti atakuwa mfalme. Huyo atayashambulia majeshi ya mfalme wa kaskazini na kuingia katika ngome zao na kushinda.
8 Atazibeba sanamu za kusubu za miungu yao na vyombo vya thamani vya fedha na dhahabu mpaka nchini Misri. Kwa muda wa miaka kadhaa, mfalme wa kusini hatamshambulia mfalme wa kaskazini.
9 Lakini baadaye, mfalme huyu wa kaskazini atauvamia ufalme wa kusini, ila atalazimika kurudi katika nchi yake.
10 “ ‘Wana wa mfalme wa kaskazini watakusanya jeshi kubwa na kujiandaa kwa vita. Jeshi hilo litasonga mbele kama mafuriko litapita na kupigana vita mpaka ngome ya adui.
11 Hapo, mfalme wa kusini, kwa hasira yake, atapigana vita na mfalme wa kaskazini ambaye naye atamkabili kwa jeshi kubwa, lakini litashindwa.
12 Baada ya kulishinda vibaya jeshi la kaskazini na kuua maelfu, ataanza kujisifu, ila hataendelea kuwa mshindi.
13 “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi.