1 “ ‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa.
2 Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele.
3 Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele.
4 Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”
5 “Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.
6 Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe?