2 Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele.
3 Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele.
4 Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”
5 “Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.
6 Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe?
7 Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’
8 Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’