4 Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”
5 “Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.
6 Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe?
7 Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’
8 Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’
9 Akanijibu, ‘Danieli, sasa nenda zako, kwani maneno haya ni siri na yamefungwa kwa kutiwa mhuri mpaka wakati wa mwisho.
10 Watu wengi wataondolewa uchafu, watatakaswa na kusafishwa. Lakini watu waovu wataendelea kutenda uovu. Hakuna hata mmoja wa hao waovu atakayeelewa; wenye hekima ndio watakaoelewa.