17 Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme.
18 Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”
19 Hapo, mfalme Nebukadneza akawaka hasira, sura yake ikabadilika kwa chuki dhidi ya Shadraki, Meshaki na Abednego. Akaamuru mwako wa moto wa tanuri uongezwe mara saba kuliko kawaida yake.
20 Akaamuru watu fulani wenye nguvu kabisa katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa katika ile tanuri ya moto mkali.
21 Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali.
22 Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.
23 Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali.