21 majani yake yakiwa mazuri, na matunda yake mengi ya kulisha viumbe vyote, wanyama wa porini wakipata kivuli chini yake, na ndege wa angani wakikaa katika matawi yake,
22 basi, ni wewe ee mfalme ambaye umekuwa mkubwa na mwenye nguvu. Ukuu wako umefika mpaka mbinguni, na ufalme wako umeenea mpaka miisho ya dunia.
23 Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’
24 “Hii basi, bwana wangu, ndiyo maana ya ndoto yako, kadiri ya uamuzi wa Mungu Mkuu juu yako:
25 Wewe utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini, utakula majani kama ng'ombe; utalowa kwa umande wa mbinguni. Utakaa katika hali hiyo kwa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.
26 Tena amri ile ya kukiacha kisiki na mizizi ya mti huo ardhini ina maana hii: Wewe utarudishiwa tena ufalme wako hapo utakapotambua kwamba Mungu wa mbinguni ndiye atawalaye.
27 Kwa sababu hiyo, ee mfalme, sikiliza shauri langu. Achana na dhambi zako na maovu yako, utende haki na kuwaonea huruma waliodhulumiwa; huenda muda wako wa fanaka ukarefushwa!”