29 Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme Nebukadneza alikuwa anatembea juu ya dari ya ikulu ya mji wa Babuloni.
30 Basi, akasema kwa sauti, “Tazama Babuloni, mji mkuu nilioujenga kwa nguvu zangu uwe makao yangu ya kifalme na kwa ajili ya utukufu wangu!”
31 Mara tu alipotamka maneno hayo, sauti kutoka mbinguni ikatamka: “Ewe mfalme Nebukadneza, sikiliza ujumbe huu juu yako! Ufalme umekutoka!
32 Utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini kondeni, na utakula majani kama ng'ombe! Utakaa katika hali hiyo kwa muda wa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.”
33 Mara moja jambo hilo juu ya mfalme Nebukadneza likatekelezwa. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alilowa kwa umande wa mbinguni, na nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, na kucha zake kama za ndege.
34 “Mwishoni mwa ile miaka saba, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kutazama juu mbinguni na akili zangu zikanirudia. Nilimshukuru Mungu Mkuu na kumheshimu yeye aishiye milele:Kwa sababu enzi yake ni enzi ya milele,ufalme wake wadumu kizazi hata kizazi.
35 Wakazi wote wa dunia si kitu;hufanya atakavyo na viumbe vya mbinguni,na wakazi wa duniani;hakuna awezaye kumpinga,au kusema ‘Unafanya nini?’