Danieli 9:21-27 BHN

21 yule mtu Gabrieli, ambaye nilikuwa nimemwona katika maono hapo awali, alishuka kwa haraka mpaka mahali nilipokuwa. Ilikuwa wakati wa kutoa sadaka ya jioni.

22 Basi, akaniambia, ‘Danieli, nimekuja kukupa hekima na uwezo wa kufahamu.

23 Ulipoanza kuomba, Mungu alitoa jibu, nami nimekuja kukueleza jibu hilo kwa kuwa unapendwa sana. Kwa hiyo, usikilize kwa makini jibu hilo na kuelewa maono hayo.

24 “ ‘Muda wa miaka saba mara sabini umewekwa kwa ajili ya watu wako na juu ya mji wako mtakatifu ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kusamehe uovu, kuleta haki ya milele, kutia mhuri maono na unabii na kupaka mafuta mahali patakatifu kabisa.

25 Basi, ujue na kufahamu jambo hili: Tangu wakati itakapotolewa amri ya kujengwa upya mji wa Yerusalemu hadi kuja kwake aliyepakwa mafuta, yule aliye mkuu, ni muda wa majuma saba. Kwa muda wa majuma sitini na mawili, mji wa Yerusalemu utajengwa upya, wenye barabara kuu na mahandaki, lakini wakati huo utakuwa wa taabu.

26 Baada ya majuma hayo sitini na mawili, yule aliyepakwa mafuta atakatiliwa mbali hatabaki na kitu. Mji na mahali patakatifu kabisa vitaharibiwa na jeshi la mtawala atakayekuja kushambulia. Mwisho wake utafika kama mafuriko, kukiwa na vita na maangamizi kama yalivyopangwa na Mungu.

27 Mtawala huyo atafanya mapatano imara na watu wengi kwa muda wa miaka saba. Baada ya nusu ya muda huo atakomesha tambiko na sadaka. Mahali pa juu hekaluni patasimamishwa chukizo haribifu, nalo litabaki hapo mpaka yule aliyelisimamisha atakapoangamizwa kama ilivyopangwa na Mungu.’”