3 Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu.
4 Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema:“Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako.
5 Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako.
6 Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako waliongea na wafalme wetu, wakuu wetu, wazee wetu na taifa letu lote.
7 Kwako, ee Bwana, kuna uadilifu, lakini sisi daima tumejaa aibu. Jambo hili ni kweli kwetu sote tuishio Yudea, wakazi wa mji wa Yerusalemu na Waisraeli wote ambao umewatawanya katika nchi za mbali na za karibu kwa sababu ya kukosa uaminifu kwako.
8 Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea.
9 Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi.