1 Baada ya mambo hayo, mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani, akawa waziri mkuu. Hamani alikuwa mwanawe Hamedatha, na wa uzao wa Agagi.
2 Mfalme aliamuru maofisa wote wa serikali yake wamtii Hamani kwa kumwinamia na kumsujudia. Lakini Mordekai, hakumwinamia wala kumsujudia.
3 Maofisa kadhaa wa mfalme waliokuwa penye lango la mfalme, wakamwuliza Mordekai, “Mbona wewe waidharau amri ya mfalme?”
4 Kila siku walimshauri aache tabia hiyo, lakini Mordekai hakukubaliana nao. Alikataa kufanya hivyo kwa madai kwamba yeye ni Myahudi na kwa hiyo hawezi kumsujudia Hamani. Basi, wakamwarifu Hamani ili waone kama ataivumilia tabia ya Mordekai.
5 Hamani aliwaka hasira alipojua kwamba Mordekai hamwinamii wala hamsujudii.