Esta 5 BHN

Esta awaalika mfalme na Hamani karamuni

1 Siku ya tatu ya mfungo wake, Esta alivalia mavazi yake ya kimalkia, akaenda akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuelekea ukumbi wa mfalme. Mfalme alikuwamo ndani, amekaa katika kiti chake cha enzi, kuelekea mlango wa nyumba ya mfalme.

2 Mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, alipendezwa naye, akamnyoshea fimbo ya dhahabu aliyokuwa ameshika mkononi mwake. Esta akakaribia, akagusa ncha ya fimbo.

3 Hapo mfalme akauliza, “Unataka nini Esta? Niambie unachotaka, nawe utapata – hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”

4 Esta akamjibu, “Ukipenda, ewe mfalme, uje leo pamoja na Hamani, kwenye karamu ninayoandaa kwa ajili yako, mfalme.”

5 Mfalme akatoa amri Hamani aje upesi, kama Esta alivyoomba. Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu aliyoandaa Esta.

6 Walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta: “Unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.”

7 Esta akamjibu, “Ombi langu ni hili:

8 Kama u radhi, ewe mfalme, kukubali ombi langu, basi, naomba wewe na Hamani mje kesho kwenye karamu nyingine nitakayowaandalieni. Wakati huo nitakujulisha ombi langu.”

Hamani apanga kumuua Mordekai

9 Hamani alitoka huko karamuni mwenye furaha tele na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai penye lango la ikulu, hasimami wala hampi heshima, Hamani akawaka hasira.

10 Hata hivyo, alijizuia, akaenda zake nyumbani. Halafu akawaalika nyumbani kwake rafiki zake, na kumwomba Zereshi mkewe ajiunge nao.

11 Ndipo akaanza kuelezea juu ya utajiri aliokuwa nao, wana aliokuwa nao, jinsi mfalme alivyompandisha cheo, na jinsi alivyopewa madaraka zaidi kuliko maofisa wengine wote wa mfalme.

12 Hamani akaendelea kujitapa, “Isitoshe malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote pamoja na mfalme isipokuwa mimi tu. Hata kesho pia, ametualika mimi na mfalme.

13 Lakini yote haya hayaniridhishi iwapo nitaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai penye lango la ikulu.”

14 Basi, Zereshi, mkewe, na marafiki zake, wakamshauri hivi: “Kwa nini asitengenezewe mti wa kuulia, wenye urefu wa mita ishirini na mbili? Kesho asubuhi, unaweza kuzungumza na mfalme ili Mordekai auawe juu yake, kisha uende ukale karamu na mfalme kwa furaha.” Wazo hilo lilimfurahisha Hamani, naye akatengeneza mti wa kuulia.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10