1 Mordekai alipojua yote yaliyotukia, alizirarua nguo zake, akavaa vazi la gunia, na kujitia majivu. Kisha, akapita katikati ya mji akilia kwa sauti ya uchungu.
2 Alikwenda mpaka penye lango la ikulu ya mfalme, lakini hakuweza kuingia kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ikulu akiwa amevaa vazi la gunia.
3 Katika kila mkoa, mara tu amri ya mfalme ilipotangazwa, msiba mkubwa uliwakumba Wayahudi. Walifunga, wakalia na kuomboleza; na wengi wao walilala katika majivu wakiwa wamevaa magunia.
4 Malkia Esta alipoarifiwa na matowashi na watumwa wa kike wake habari za Mordekai alihuzunika sana. Akampelekea Mordekai nguo za kuvaa badala ya vazi la gunia, lakini Mordekai akazikataa.
5 Basi, akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyeteuliwa na mfalme amhudumie Esta, akamtuma kwa Mordekai kuuliza kisa na maana ya tukio hilo.
6 Hathaki alimwendea Mordekai uwanjani, mbele ya lango la ikulu.
7 Mordekai akamsimulia Hathaki yote yaliyokuwa yamempata, na kiasi kamili cha fedha ambayo Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme kama Wayahudi wote wangeangamizwa.
8 Alimpa pia nakala moja ya tangazo lililokuwa limetolewa mjini Susa kuhusu kuangamizwa kwa Wayahudi, akamwomba amchukulie Esta, amweleze hali ilivyo, na kumwambia aende kumsihi mfalme na kumwomba awahurumie Wayahudi, watu wake Esta.
9 Hathaki akaenda akamweleza Esta yote aliyosema Mordekai.
10 Naye Esta akamwambia Hathaki arudi akamwambie Mordekai,
11 “Watumishi wote wa mfalme na raia wa mikoa yote wanajua ya kwamba mtu yeyote yule akiingia katika ua wa ndani na kumwona mfalme bila kuitwa, huyo ni lazima auawe. Anayeweza kunusurika ni yule tu ambaye mfalme atamnyoshea fimbo yake ya dhahabu ili kumsalimisha. Kumbe mimi sijaitwa na mfalme, yapata mwezi mzima sasa.”
12 Mordekai alipopata ujumbe wa Esta,
13 mara alimpelekea onyo hili: “Usidhani kwamba kwa kuwa upo ikulu wewe u salama zaidi kuliko Myahudi mwingine yeyote yule.
14 Ukikaa kimya wakati kama huu, msaada utawajia Wayahudi kutoka mahali pengine, nao wataokolewa; lakini wewe utakufa, na jamaa ya baba yako itaangamia. Ni nani ajuaye pengine umefanywa malkia kwa ajili ya wakati kama huu!”
15 Esta alimpelekea Mordekai jibu hili:
16 “Nenda ukawakusanye pamoja Wayahudi wote waliopo mjini Susa. Fungeni, msile wala msinywe kwa siku tatu, usiku na mchana, kwa ajili yangu. Na mimi na watumwa wa kike wangu tutafanya vivyo hivyo. Kisha, nitamwendea mfalme, ingawa ni kinyume cha sheria. Kama ni kuuawa, na niuawe.”
17 Basi, Mordekai akaenda zake na kufanya kama Esta alivyomwambia.