10 Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi.
11 Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.”
12 Basi, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza, Hamani aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawapa tangazo ambalo alitaka litafsiriwe kwa kila lugha na kila namna ya maandishi katika utawala huo, halafu nakala zisambazwe kwa watawala wote, wakuu wa mikoa yote, na viongozi wa makabila – kufuatana na lugha zinazotumika kwao. Tangazo hilo lilitolewa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kupigwa mhuri kwa pete yake.
13 Matarishi walizipeleka nyaraka hizo kwa kila mkoa katika utawala huo. Tangazo hilo lilisema kwamba kwa siku moja tu, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari, Wayahudi wote – vijana kwa wazee, wanawake kwa watoto, wote lazima wauawe, waangamizwe na kufutiliwa mbali, na mali zao zote zichukuliwe.
14 Taarifa hiyo ilitakiwa iandikwe hadharani katika kila mkoa, ili kila mtu ajiandae kwa ajili ya siku hiyo.
15 Kwa amri ya mfalme, tangazo hili lilitolewa katika mji mkuu wa Susa, nao matarishi wakalitangaza katika mikoa yote. Mfalme na Hamani walikaa chini kunywa wakati watu mjini Susa wanafadhaika.