11 Basi, Hamani akachukua mavazi hayo na kumvisha Mordekai, akamtembeza kwenye uwanja wa mji akiwa juu ya farasi wa mfalme, huku anatangaza: “Hivi ndivyo anavyotendewa mtu ambaye mfalme amependa kumpa heshima.”
12 Kisha Mordekai akarudi kwenye lango la ikulu. Lakini Hamani akakimbilia nyumbani kwake, amejaa huzuni na amekifunika kichwa chake kwa aibu.
13 Huko akawasimulia Zereshi, mkewe, na rafiki zake wote mambo yote yaliyompata. Zereshi na hao rafiki zake wakamwambia: “Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kupoteza madaraka yako kwake ni wa kabila la Wayahudi, basi, hutamweza; atakushinda kabisa.”
14 Walipokuwa bado wanaongea hayo, matowashi wa mfalme wakafika hima kumchukua Hamani kwenda kwenye karamu ya Esta.