20 Ukihitaji kitu kingine chochote kwa ajili ya nyumba ya Mungu wako unaweza kukipata kutoka katika hazina ya mfalme.
21 Mimi mfalme Artashasta, natoa amri kwa waweka hazina wote katika mkoa wa magharibi ya mto Eufrate kwamba chochote atakachohitaji Ezra, kuhani na mwandishi wa sheria ya Mungu wa mbinguni, mtampa, tena bila kusita,
22 fedha kiasi atakacho mpaka kufikia kilo 3,400, ngano kilo 10,000, divai lita 2,000, mafuta lita 2,000, na chumvi kiasi chochote atakachohitaji.
23 Kila kitu alichoagiza Mungu wa mbinguni kwa ajili ya nyumba yake, ni lazima kitekelezwe kikamilifu, asije akaukasirikia ufalme wangu au wanangu.
24 Tunawafahamisheni pia kuwa ni marufuku kuwadai kodi ya mapato, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, walinda mlango, wafanyakazi au watumishi wengine wa nyumba hii ya Mungu.
25 Nawe Ezra, kwa kutumia hekima aliyokupa Mungu wako, hiyo uliyonayo, chagua mahakimu, na waamuzi watakaowaongoza wakazi wote wa mkoa wa magharibi ya Eufrate ambao wanaishi kufuatana na sheria ya Mungu wako. Na yule ambaye haijui sheria hiyo, mfundishe.
26 Mtu yeyote ambaye hatatii sheria ya Mungu wako na ya mfalme, na ahukumiwe mara moja: Kufa, kuhamishwa, kunyanganywa mali yake au kufungwa.”