1 Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama huku analia na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa watu wa Israeli, wanaume, wanawake na watoto, walikusanyika karibu naye wakilia kwa uchungu mwingi.
2 Ndipo Shekania, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu kwa kuoa wanawake wa kigeni wa nchi hii, lakini hata hivyo bado kuna tumaini kwa ajili ya Israeli.
3 Kwa hiyo, na tufanye agano na Mungu wetu, tuachane na wanawake hawa pamoja na watoto wao, kwa kufuatana na ushauri wako na wa wengine wanaotii amri za Mungu. Yote yatendeke kwa kufuatana na sheria.
4 Amka uchukue hatua, sisi tutakuunga mkono. Kwa hiyo jipe moyo ufanye hivyo.”
5 Ezra alianza kwa kuwafanya makuhani, viongozi, Walawi na Waisraeli wengine wote waape kwamba watafanya kama ilivyosemwa, nao wakakubali kula kiapo.
6 Kisha, Ezra akaondoka mbele ya nyumba ya Mungu, akaenda nyumbani kwa Yehohanani, mwana wa Eliashibu. Huko, Ezra alilala usiku kucha bila kula wala kunywa maji, kwa huzuni aliyokuwa nayo juu ya ukosefu wa imani ya watu waliotoka uhamishoni.
7 Tangazo lilitolewa kila mahali nchini Yuda na mjini Yerusalemu kwa wote waliotoka uhamishoni kuwa wakusanyike Yerusalemu.
8 Ikiwa mtu yeyote atashindwa kufika katika muda wa siku tatu, kulingana na amri iliyotolewa na viongozi, mali yake yote itachukuliwa, naye binafsi atapigwa marufuku kujiunga na jumuiya ya watu waliorudi kutoka uhamishoni.
9 Katika siku hizo tatu, mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walioishi katika Yuda na Benyamini walifika Yerusalemu na kukusanyika katika uwanja wa nyumba ya Mungu. Watu wote walikuwa wakitetemeka kwa sababu ya jambo waliloitiwa na kwa ajili ya mvua nyingi iliyokuwa ikinyesha.
10 Kuhani Ezra alisimama kuzungumza na watu, akawaambia: “Hamkuwa waaminifu kwa kuoa wanawake wa kigeni, na hivyo mmeiongezea Israeli hatia.
11 Sasa, tubuni dhambi zenu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na kufanya yale yanayompendeza. Jitengeni na wakazi wa nchi hii na kuwaacha wake zenu wa kigeni.”
12 Watu wote walipaza sauti na kujibu kwa pamoja, “Ni sawa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.”
13 Lakini wakaongeza kusema, “Watu ni wengi na mvua inanyesha sana. Hatuwezi kuendelea kusimama hapa uwanjani, na hili si jambo ambalo litamalizika kwa siku moja au mbili! Tumefanya kosa kubwa sana kuhusu jambo hili.
14 Afadhali maofisa wetu wabaki Yerusalemu kushughulikia jambo hili kwa niaba ya watu wote. Kisha, kila mmoja ambaye ameoa mwanamke wa kigeni na aje kwa zamu pamoja na viongozi na mahakimu wa mji wake, mpaka hapo ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapoondolewa kwetu.”
15 Hakuna aliyepinga mpango huu, ila Yonathani, mwana wa Asaheli na Yazeya, mwana wa Tikwa, nao wakaungwa mkono na Meshulamu na Mlawi Shabethai.
16 Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walikubali mpango huo, kwa hiyo kuhani Ezra aliwachagua wanaume kati ya viongozi wa koo mbalimbali na kuyaorodhesha majina yao. Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, watu hao walianza kazi yao ya uchunguzi wa jambo hilo.
17 Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, walikuwa wamekwisha maliza uchunguzi wao kuhusu wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni.
18 Hii ndiyo orodha ya wanaume waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni: Makuhani kulingana na koo zao: Ukoo wa Yeshua, mwana wa Yehosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia.
19 Hao waliahidi kuwaacha wake zao, na wakatoa kondoo dume kuwa sadaka kwa ajili ya hatia yao.
20 Ukoo wa Imeri: Hanani na Zebadia.
21 Ukoo wa Harimu: Maaseya, Elia, Shemaya, Yehieli na Uzia.
22 Ukoo wa Pashuri: Eliehoenai, Maaseya, Ishmaeli, Nethaneli, Yozabadi na Elasa.
23 Walawi: Yozabadi, Shimei, Kelaya (aliyejulikana pia kama Kelita), Pethahia, Yuda na Eliezeri.
24 Kati ya waimbaji: Eliashibu. Walinzi wa hekalu: Shalumu, Telemu na Uri.
25 Watu wengineo wa Israeli: Ukoo wa Paroshi: Ramia, Izia, Malkiya, Miyamini, Eleazari, Malkiya na Benaya.
26 Ukoo wa Elamu: Matania, Zekaria, Yehieli, Abdi, Yeremothi na Elia.
27 Ukoo wa Zatu: Eliehoenai, Eliashibu, Matania, Yeremothi, Zabadi na Aziza.
28 Ukoo wa Bebai: Yehohanani, Hanania, Zabai na Athlai.
29 Ukoo wa Bani: Meshulamu, Maluki, Adaya, Yashubu, Sheali na Yeremothi.
30 Ukoo wa Pahath-moabu: Adna, Kelali, Benaya, Maaseya, Matania, Besaleli, Binui na Manase.
31 Ukoo wa Harimu: Eliezeri, Ishiya, Malkiya, Shemaya, Shimeoni,
32 Benyamini, Maluki na Shemaria.
33 Ukoo wa Hashumu: Matenai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase na Shimei.
34 Ukoo wa Bani: Maadai, Amramu, Ueli,
35 Benaya, Bedeya, Keluhi,
36 Wania, Meremothi, Eliashibu,
37 Matania, Matenai na Yaasu.
38 Ukoo wa Binui: Shimei,
39 Shelemia, Nathani, Adaya,
40 Maknadebai, Shashai, Sharai,
41 Azareli, Shelemia, Shemaria,
42 Shalumu, Amaria na Yosefu.
43 Ukoo wa Nebo: Yeieli, Matithia, Zabadi, Zebina, Yadai, Yoeli na Benaya.
44 Wanaume hawa wote walikuwa wameoa wanawake wa kigeni. Basi wakawaacha wanawake hao pamoja na watoto wao.