1 “Yafuatayo ni masharti na maagizo ambayo mtayatimiza katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapa muimiliki, siku zote za maisha yenu nchini.
2 Haribuni kabisa mahali pote ambapo watu wanaabudu miungu yao kwenye milima mirefu, vilima na chini ya miti yenye majani mabichi.
3 Zivunjilieni mbali madhabahu zao na kuzibomoa kabisa nguzo zao. Ziteketezeni kwa moto sanamu zao za Ashera na kuzikatakata sanamu zao za kuchonga na kufutilia mbali jina lao na mahali hapo.
4 “Wala msimwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, namna hiyo yao.
5 Bali mtakwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atachagua katika makabila yote ili kuliweka jina lake na makao yake hapo; huko ndiko mtakakokwenda.