1 “Mtu akipatikana ameuawa mbugani katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni muimiliki, nanyi hamjui ni nani aliyemuua,
2 wazee na waamuzi wenu watajitokeza na kupima umbali wa kutoka mahali maiti ilipo hadi miji ya karibu.
3 Kisha, wazee wa mji ule ulio karibu zaidi na ile maiti watachukua ndama ambaye hajatumiwa kufanya kazi yoyote ile wala kutiwa nira.
4 Nao watamteremsha ndama bondeni kwenye kijito ambacho hakikauki, na bonde hilo halilimwi au kupandwa; huko watamvunja huyo ndama shingo.
5 Nao makuhani wa ukoo wa Lawi sharti wawepo hapo. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwachagua wamhudumie na kubariki watu kwa jina lake. Wao pia ndio wenye mamlaka kuhusu kila tukio na utumiaji wa nguvu.
6 Yule ndama atakapovunjwa shingo, wazee wote wa mji huo ulio karibu na mtu huyo aliyeuawa, watanawa mikono yao kwa maji juu ya ndama
7 na kusema, ‘Hatuna hatia kuhusu kifo hiki, wala hatumjui aliyemuua.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, uwasamehe watu wako wa Israeli ambao umewakomboa, usiwawekee watu wako Israeli hatia ya mauaji ya mtu asiye na hatia, ila uwasamehe hatia hiyo.’
9 Hivyo damu hiyo iliyomwagwa haitakuwa tena sababu ya lawama kwenu, maana mmefanya yale Mwenyezi-Mungu aliyotaka myafanye.
10 “Mkienda kupigana vita na adui, naye Mwenyezi-Mungu akawapeni ushindi, mkawachukua mateka,
11 kama mmoja wenu akiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri, akamtamani na kutaka kumwoa,
12 basi, wewe mwanamume mhusika utamchukua nyumbani kwako, naye atanyoa kichwa chake, akakate kucha zake,
13 na kubadili nguo zake za mateka. Atakaa muda wa mwezi mzima kumwombolezea baba yake na mama yake; kisha waweza kumwoa uwe mume wake, naye awe mke wako.
14 Kama baadaye hupendezwi naye, utamwacha huru aende zake; usimwuze kwa fedha, wala usimfanye kama mtumwa, kwa sababu ulimnyenyekesha.
15 “Ikiwa mwanamume fulani ana wake wawili naye anampenda mmoja kuliko mwingine. Nao wanawake hao wamemzalia watoto wa kiume, na mtoto wa kwanza kuzaliwa ni wa yule mama asiyempenda,
16 ikafika siku ya kuwapa hao wanawe urithi, huyo baba haruhusiwi kamwe kumtendea mtoto wa yule mke anayempenda kama kwamba ni mtoto mzaliwa wa kwanza, badala ya yule mtoto wa mama asiyependwa ambaye ndiye aliye mzaliwa wa kwanza.
17 Lazima amkubali yule mzaliwa wa kwanza, mtoto wa yule mwanamke asiyependwa, na kumpa haki yake: Sehemu ya mali zake mara mbili.
18 “Kama mtu ana mtoto mkaidi na mtundu, asiyemtii baba yake au mama yake wanapompa nidhamu,
19 basi, mama na baba yake huyo mtoto watamchukua mlangoni mwa nyumba anamoishi na kumpeleka kwa wazee katika lango la mji.
20 Wazazi hao watawaambia wazee wa mji: ‘Mtoto wetu ni mkaidi na mtundu, hataki kutusikiliza, ni mlafi na mlevi.’
21 Hapo watu wa mji huo watampiga mawe mtoto huyo mpaka afe. Ndivyo mtakavyokomesha ubaya huo miongoni mwenu. Kila mtu katika Israeli atasikia tukio hilo na kuogopa.
22 “Kama mtu amefanya kosa la jinai linalompasa auawe na akauawa kwa kutundikwa mtini,
23 maiti yake isiachwe mtini usiku wote, bali mtaizika siku hiyohiyo. Maana mtu aliyenyongwa amelaaniwa na Mungu nanyi hamtaitia najisi nchi yenu mliyopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, iwe mali yenu.